Ijumaa, 11 Novemba 2016

LUCKY DUBE: Kutoka mtunza bustani hadi mkali wa reggae



LUCKY Dube si jina geni miongoni mwa wapenzi wa muziki duniani kote ambapo pamoja na ukweli kwamba kwa sasa hayupo nasi baada ya kufariki Dunia Oktoba 18, 2007, lakini hadi sasa kazi zake za muziki wa reggae zimekuwa zikitamba, zikiimbwa katika mikusanyiko mbalimbali, zikiwamo kumbi za starehe.

Kati ya mambo yanazozifanya kazi zake kuendelea ‘kuishi’, ni ujumbe uliomo ambao wakati mwingine umekuwa ukiliwadha kama si kufariji pale yeyote alipokuwa na majonzi, lakini pia midundo yake ikiwa ni burudani tosha.

Unapopita katika mitaa mbalimbali jijini Dar es Salaam na kwingineko nchini, Afrika na hata Ulaya na Amerika, huwezi kumaliza siku mbili bila kusikia wimbo wa Lucky Dube au bango lenye picha au ujumbe uliomo katika moja ya kazi zake.

Miongoni mwa nyimbo za mkali huyo zilizowahi kutamba na zikiendelea kufanya hivyo hadi sasa, ni Big Boys Don’t Cry, Born To Suffer, Release Me, Ratas Never Die, The Other Side, Trinity, War And Crime, Love Me, Truth In The World, Different Colours, Together As One, Back To My Roots, I Want To Know Whats Love Is, Prisoner, It’s Not Easy, I’ve Got You Baby, Remember Me, House Of Exile na nyinginezo nyingi.

Lucky Dube ni nani?

Lucky Philip Dube ni mkali wa muziki wa reggae wa Afrika Kusini aliyezaliwa Agosti 3, mwaka 1964 katika Mji wa Ermelo, zamani ukijulikana kama Eastern Transvaal, kwa sasa Mpumalanga, kabla ya kukutwa na mauti jioni ya Oktoba 18, 2007 kwa kushambuliwa kwa kupigwa risasi jijini Johannesburg katika eneo la Rosettenville.


Akiwa kama Rastafarian, kabla ya kukutwa na mauti, alifanikiwa kurekodi albamu 22 katika ludha za Kizulu, Kiingereza na Kiafrikana ndani ya miaka yake 25 na ndiye aliyekuwa mwanamuziki aliyeuza zaidi kazi zake za muziki nchini humo.

Wazazi wake walitengana kabla ya kuzaliwa kwake ambapo alilelewa na mama yake pekee aliyempa jina la Lucky akimaanisha kuwa kuzaliwa kwake kulikuwa kwa bahati baada ya mimba zake kadhaa kuharibika.

Akiwa na ndugu zake wawili, Thandi na Patrick, Dube alitumia muda wake mwingine wa utotoni akiwa na bibi yake, Sarah, wakati mama yake akiwa kazini. Mwaka 1999 alifanya mahojiano na kumwelezea bibi yake huyo kama ‘mtu anayempenda zaidi’ ambaye “alifanya mambo mengi kuniwezesha kuwa kama nilivyo leo.” 

Alivyoanza muziki

Akiwa mtoto, Dube alikuwa akifanya kazi ya kutunza bustani lakini kadri alivyokua, alibaini kuwa hakuwa akipata fedha za kutosha kuilisha familia yake, hapo ndipo alipoamua kwenda shule.

Alipokuwa shule, alijiunga na kwaya, akiwa pamoja na baadhi ya rafiki zake, na kuunda kundi lake la kwanza la muziki, lililoitwa The Skyway Band.

Akiwa shuleni, alibaini harakati za Rastafari. Akiwa na umri wa miaka 18, Dube aliungana na bendi ya binamu yake, The Love Brothers, iliyokuwa ikicheza muziki wa aina ya pop ya Kizulu iliyojulikana kama mbaqanga, huku akiendesha maisha yake kwa kufanya kazi katika kampuni ya Hole and Cooke akiwa kama mlinzi katika moja ya yadi za magari iliyopo Midrand.
 
Bendi hiyo ilisaini mkataba na kampuni ya kurekodi muziki iliyofahamika kama Teal Record Company, iliyokuwa chini ya Richard Siluma (Teal baadaye ilishirikiana na kampuni ya Gallo Record).

Japo Dube alikuwa bado yupo shule, bendi hiyo ilikuwa ikirekodi kazi zao jijini Johannesburg wakati shule zikiwa zimefungwa. Matokeo yake albamu zilitolewa chini ya jina la Lucky Dube na Supersoul. Albamu ya pili ilitolewa muda mfupi baadaye, na safari hii Dube aliandika baadhi ya mashairi pamoja na kuimba. Ulikuwa ni wakati huu ambao alianza kujifunza Kiingereza.

Kuhamia kwenye reggae

Katika albamu yao ya tano ya Mbaqanga, Dave Segal (ambaye baadaye alikuja kuwa mhandisi wa sauti wa Dube) alijiunga naye na kutao kitu kilichokwenda kwa jina la ‘Supersoul’. Albamu zote hizo zilirekodiwa kwa jina la Lucky Dube.

Kwa wakati huo, Dube alianza kujikusanyia mashabiki ambao walikuwa wakimuunga mno mkono na kuvutiwa naye, hasa kutokana na umahiri wake katika kuimba nyimbo za reggae wakati wa matamasha ya moja kwa moja ‘live’.

Akiwa amepata hamasa kutoka kwa wakali wa reggae Jimmy Cliff na Peter Tosh, alianza kuachana na muziki wake wa awali na kuhamia ule wa reggae ya asili ya kijamaica ambao ulikuwa umejizoea umaarufu mno nchini Afrika Kusini kwa wakati huo.

Aliamua kujaribu kujikita moja kwa moja kwenye muziki huo na mwaka 1984, alitoa albamu aliyoipa jina la Rastas Never Die. Rekodi hiyo haikuza sana ambapo ilikuwa ni nakala 4000 tu ukilinganisha na nakala 30,000 za albamu ya mbaqanga.

Albamu yake hiyo iliyokuwa ikihamasisha harakati za kupinga ubaguzi wa rangi, ilifungiwa mwaka 1985, kwasababu ya baaadhi ya mashairi yake tata, mfano katika wimbo wa ‘War and Crime’.

Hatahivyo, hakukata tama na kuendelea kufanya muziki wa reggae moja kwa moja (live) katika majukwaa mbalimbali ambapo mwisho wa siku, aliachia albamu yake ay pili ya reggae.

‘Think About The Children’ ya mwaka 1985 ambayo ilipata mafanikio makubwa kwa kuuza nakala lukuki na kumtambulisha Dube kama msanii maarufu wa reggae nchini Afrika Kusini ambapo alivutia mashabiki lukuki hata nje ya nchi yake, ikiwamo hapa Tanzania.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni